Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 10 mwaka huu) ili kupitia
na kutoa uamuzi/ushauri kwa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele
yake.
Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao
hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba,
Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
Suala
la ugombea wa Michael Wambura katika FAMMichael Wambura aliomba uongozi
katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM) katika uchaguzi
uliofanyika Novemba mwaka jana.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo. Wambura
hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya
TFF. Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya
kushughulikia shauri hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati
ya Rufani ya TFF ambayo ilimpa haki ya kugombea.
Kutokana
na mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa
mwisho katika masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa
Kamati ya Rufani kuhusu uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya
TFF iliomba mwongozo wa kisheria kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi
za Wachezaji.
Kwa vile Kamati hizo mbili (Uchaguzi na
Rufani) haziko katika mtiririko wa moja kwa moja wa utoaji maamuzi,
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliishauri Sekretarieti
ya TFF kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ili
kupata muongozo juu ya suala hilo.
Katika muongozo wake,
FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF chombo cha mwisho cha
rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF ni Kamati ya
Uchaguzi ya TFF.
Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si
vizuri chombo kimoja kikawa msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena
ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi kwenye uchaguzi husika.
Hivyo,
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo
mawili kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili
kiwepo chombo kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa
Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Mapendekezo hayo ni; Iundwe
Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote zinazotokana na uamuzi
uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF
isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani zinazotokana na uchaguzi
wa wanachama wa TFF. AU. Rufani zote zinazotokana na uchaguzi wa
wanachama wa TFF zisikilizwe na Kamati ya Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo
Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo kiwe chombo cha mwisho kwa wasiokubaliana
na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.Inatoka kwa mdau.
No comments:
Post a Comment