Twite alitua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam saa tisa alasiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda na kupokewa na viongozi wa Yanga pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.
Aliyeongoza mapokezi ya beki huyo wa zamani wa APR ya Rwanda ni makamu mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Seif Ahmed Magari na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa.
Awali, ujio wa beki huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ulionekana kama sinema, kwani licha ya ndege kutua uwanjani mapema huku mashabiki wakimsubiri kwamba hamu kubwa, alichelewa kutoka nje ya uwanja huo.
Na pale alipotoka nje, alikuwa ameongozana na Mwesigwa pamoja na Seif huku wakiwa wamezungukwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo maarufu kwa jina la makomandoo.
Beki huyo alikuwa amevalia kaptura ya khaki na fulana ya njano, lakini mara baada ya kutoka nje, baadhi ya mashabiki walimvisha jezi nyingine yenye rangi ya njano na kijani, ikiwa na namba nne na jina la Rage mgongoni.
Jezi hiyo ilikuwa na jina la Rage, kufuatia msuguano mkali kati ya klabu hiyo na Simba kuhusu usajili wa beki huyo, ambapo awali ilidaiwa kuwa, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alishafanya naye mazungumzo na kumsajili kwa kitita cha dola 30,000 za Marekani, zaidi ya sh. milioni 35.
Lakini baadaye kukawa na taarifa kwamba, beki huyo alighairi kujiunga na Simba, badala yake akaingia mkataba na Yanga baada ya kulipwa kitita cha sh. milioni 75.
Tayari Twite ameshakamilisha taratibu zote za kujiunga na Yanga ikiwa ni pamoja na kupatiwa hati ya uhamisho ya kimataifa (ITC) kutoka APR.
Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo, Twite alisema amekuja Tanzania kucheza soka na aliwataka mashabiki wa Yanga watarajie mambo makubwa kutoka kwake.Inatoka kwa mdau.
No comments:
Post a Comment