MWANADADA Rachel Haule ‘Recho’ amekiri kuwa, tangu alipoanza kuishi na mchumba wake, George Saguda, maisha yake yamebadilika.
Mchezaji
filamu huyo machachari alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa,
maisha ya kuwa msela na kuishi na mwenza wako yana tofauti kubwa.
“Tangu nilipoanza kuishi na Saguda, nimeona mabadiliko makubwa kimaisha,”alisema msanii huyo mwenye umbo lililojaa vyema.
Saguda ni mmoja wa watayarishaji mahiri wa filamu nchini na alianza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Recho mapema mwaka huu.
“Nampenda sana Saguda kwa sababu kwa sasa yeye ni msaada kwangu kiushauri, kimawazo na kimaisha,” alisema Recho.
“Naweza
kusema Saguda kanituliza kwani kwa sasa siwezi kufanya jambo lolote la
kimaendeleo bila kushauriana na mwenzangu, tofauti na awali ambapo
nilikuwa najiamulia kitu cha kufanya na hakuna wa kuniuliza,”aliongeza.
Kwa
sasa, Recho na Saguda wapo katika mipango ya kufunga ndoa ili kuwa mume
na mke.Recho ni mwenyeji wa mkoa wa Ruvuma na wakati alipojitosa kwenye
fani hiyo, alikuwa akisakamwa na shutuma nyingi kuhusu aina ya mavazi
aliyokuwa akivaa.
Mwanadada
huyo mantashau alikiri kuwa, baada ya kuwepo kwenye gemu kwa muda
mrefu, alijikuta akibadilika taratibu na hatimaye kuanza kuvaa mavazi ya
staha.
“Unajua
baada ya kufika mjini, nilitekwa na mji na nilikuja kucharuka zaidi
baada ya kuanza kufahamiana na wasanii wa bongo movi, ambao mara zote
walikuwa wakinishauri nivae nguo fupi ili kuleta mvuto zaidi,”alisema.
Recho
alisema inawezekana kwa wakati huo alikuwa akijiona hana tatizo, lakini
kutokana na tasnia ya bongo movi kukumbwa na matatizo mengi, naye
alijikuta akiingizwa kwenye mkumbo.
“Sio
kwamba nilitaka kuharibiwa, hapana, nilijikuta tu napenda kuvaa mavazi,
ambayo rafiki zangu walikuwa wakiyavaa na kadri siku zilivyokuwa
zinakwenda, nilizidi kuzoea,” alisema.
Mwanadada
huyo alikiri kuwa, fani ya filamu imemwezesha kupata mafanikio makubwa
kimaisha, ikiwa ni pamoja na kumtangaza na kumfanya ajulikane zaidi hapa
nchini.Baadhi ya filamu alizoshiriki kuzicheza ni pamoja na Cindy, Life
to Life, Loreen, Men’s Day Out na Unpredictable.
Amemtaja
msanii Blandina Chagula ‘Johari’ kuwa ni miongoni mwa watu waliomfanya
avutike kujitosa kwenye fani hiyo kutokana na kuvutiwa na uigizaji wake.
Recho
alikanusha madai ya kuwepo kwa rushwa ya ngono kwenye tasnia ya filamu.
Alisema inawezekana jambo hilo lipo, lakini tangu alipojitosa kwenye
fani hiyo, hajawahi kukumbana na adha hiyo.
“Maprodyuza ambao nimefanya nao kazi, wanaangalia uwezo wangu na kunikubali,” alisema.
Recho
amekiri kuwa, mara ya kwanza alipopewa nafasi ya kucheza filamu ya
Mtoto wa geti kali, alipata wakati mgumu baada ya kutakiwa ampige busu
mwigizaji mwenzake wa kiume na lionekane busu la kweli.
“Nilisumbuka mno. Ilikuwa changamoto kubwa na kusema kweli nilimsumbua sana muongozaji wa filamu hiyo,”alisema.
“Ikitokea
kuna eneo ambalo natakiwa kumpa denda msanii mwenzangu kwa ajili ya
kuonesha uhalisia, nitafanya hivyo kwa ajili ya sanaa lakini baada ya
hapo hakuna kinachoweza kuendelea kwa sababu nina mtu wangu,
tunapendana,” alisisitiza.
Recho
alisema amekuwa akifanya mazoezi kila siku kwa lengo la kuutuza mwili
wake. Alisema amekuwa akiamka saa 11:30 asubuhi na kila ifikapo saa
12:00, anakuwa mazoezini kwenye viwanja vya klabu ya Leaders, Kinondoni,
Dar es Salaam.
Mwanadada huyo anapenda sana kula wali kwa maharage, muziki na kwenda kujirusha klabu. Ndoto zake kubwa ni kuwa mbunge ili aweze kuwatetea wanawake wenzake.
No comments:
Post a Comment