UTANGULIZI:
1.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko makubwa
kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten,
mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.
2. Mwangosi ambaye pia alikuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Iringa (IPC),
aliuawa akiwa kazini jana, Septemba 2, 2012, wakati polisi walipokuwa
wakiwadhibiti wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
3. Tukio hili linaiingiza
Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji wa uhuru wa
habari, kwani ni kwa mara ya kwanza tunashuhudia mwandishi wa habari
AKIUAWA WAKATI AKITEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA KIHABARI.
4. Taarifa za awali zinaonyesha
kuwa Mwangosi kabla ya kufikwa na mauti saa 9.30 alasiri katika kijiji
cha Nyololo, Mufindi, alizingirwa na kushambuliwa na polisi waliokuwa
katika eneo la tukio. Na hata alipopiga kelele za kuomba msaada,
hakusikilizwa na matokeo yake aliuawa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni
bomu.
5. Kwa kushirikiana na Baraza la
Habari Tanzania, TEF tumechukua hatua za haraka za kuunda timu ya
uchunguzi wa suala hilo, ambayo itakwenda mkoani Iringa mapema kadri
itakavyowezekana, ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Lengo la uchunguzi
huo ni kuweka kumbukumbu sahihi (documentation) ya tukio hilo la aina
yake katika historia ya nchi yetu.
6. Matokeo ya uchunguzi huo
pamoja na mwingine unaofanywa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari
Tanzania (UTPC), ndiyo yatakayotoa mwelekeo wa hatua ambazo TEF
itachukua dhidi ya Jeshi la Polisi katika siku chache zijazo.
No comments:
Post a Comment