skills za kitaa

Monday, July 22, 2013

Kajala Afunguka

KAJALA ATOA YA MOYONI



MSANII nyota wa filamu nchini, Kajala Masanja amewatahadharisha wasanii wenzake wa kike wawe makini wanapoanzisha uhusiano wa kimapenzi na wanaume.

Kajala amesema kutokuwa kwake makini kumchunguza mumewe, Faraja Chambo kabla ya kufunga naye ndoa, ndiko kulikomponza na kujikuta akijumuishwa katika kesi ya kutakatisha pesa.

Msanii huyo aliyenusurika kufungwa jela miaka saba, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mboni Show, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.

"Tusikurupuke, tuwachunguze wanaume zetu kabla ya kuanzisha nao uhusiano wa kimapenzi. Hapa nilipo sitaki tena mwanaume,"alisema.

Kajala alikiri kuwa, baada ya kuachana na mpenzi wake wa zamani, P Funky Majani, ambaye alidumu naye kwa zaidi ya miaka sita, alichanganyikiwa na kujitosa kimapenzi kwa mumewe bila kumchunguza.

"Nilichojua ni kwamba alikuwa anafanyakazi benki, mambo mengine muhimu sikuyachunguza,"alisema.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ilimtia hatiani Kajala katika makosa mawili na kumuhukumu kwenda jela miaka saba ama kulipa faini ya sh. milioni 13. Kajala alilipiwa faini hiyo na msanii mwenzake wa filamu Wema Sepetu.

Mumewe, Faraja alipatikana na hatia katika makosa matatu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 12 jela ama kulipa faini ya sh. milioni 200. Tayari Faraja ameshaanza kutumikia kifungo hicho.

Kajala alisema hakutarajia katika maisha yake iwapo ingetokea siku Wema angejitolea kumlipia faini ya sh. milioni 13 ili kumnusuru kwenda jela.

"Mimi na Wema tulikuwa marafiki, lakini wakati napelekwa Segerea, hatukuwa tukizungumza, tulikuwa tumegombana. Lakini wakati nikiwa mahabusu, alikuja kunitembelea, tukazungumza na kumaliza tofauti zetu,"alisema Kajala.

"Wema ni mmoja wa wasanii waliokuwa wakija mara kwa mara kunitembelea Segerea. Wakati mwingine alipokuwa akija, askari wa magereza walikuwa wakimzuia kuniona, sielewi kwa nini,"aliongeza.

Kajala alisema siku alipohukumiwa kwenda jela ama kulipa faini, alilia kwa uchungu kwa sababu aliamini mwisho wake umefika. Alisema alianza kupata faraja baada ya wasanii, Mahsen Awadh 'Dk. Cheni' na Elizabeth Michael 'Lulu' walipomfuata na kumueleza kwamba, Wema amekwenda benki kuchukua fedha za kumlipia faini.

Msanii huyo alisema si kweli kwamba fedha alizozitoa Wema zilitoka kwa watu wengine. Alisema anachoamini ni kwamba, fedha zile zilikuwa za Wema na alikwenda kuzitoa katika akaunti yake benki.

Kajala alisema pia kuwa, si kweli kwamba amepewa masharti na Wema ya kulipa fedha hizo kupitia filamu mbalimbali atakazozicheza. Alisema hakuna masharti hayo kati yake na Wema.

Kutokana na kuthamini msaada huo wa Wema, Kajala alisema ameamua kuchora tattoo yenye jina la msanii huyo kwenye bega lake la mkono wa kiume. Alisema hatarajii kuifuta tattoo hiyo hata kama atagombana na Wema katika siku zijazo.

"Nimechora tattoo ya Wema kwa sababu namuonyesha jinsi gani namshukuru na kukithamini kitu alichonifanyia,"alisema Kajala na kusisitiza kuwa, tattoo hiyo itabaki daima kwenye bega lake vyovyote itakavyokuwa.

Kajala alisema amejifunza mengi kutokana na kuishi jela kwa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kurekebisha mwenendo wa maisha yake. Alisema Kajala wa sasa si yule wa zamani.

"Kabla ya kupatwa na matatizo haya, nilikuwa nikichukulia kila kitu rahisi rahisi. Nilikuwa natoka matembezini hovyo na kufanya lolote ninalotaka. Kwa sasa sifanyi tena mambo hayo. Nimeamua kutulia na familia yangu kwa sababu ndiyo iliyonithamini wakati wa matatizo,"alisema Kajala.

Kwa mujibu wa Kajala, alikuwa karibu na Lulu walipokuwa pamoja gereza la Segerea, ikiwa ni pamoja na kushiriki kufanya ibada kwa lengo la kumuomba Mungu awanusuru katika kesi zilizokuwa zikiwakabili.

Alisema kamwe hakuwahi kupata nafasi ya kutoka gerezani nyakati za usiku na kwenda kutanua kwenye klabu za burudani kama ilivyowahi kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari. Alisema habari hizo zilikuwa za uzushi.

Kajala alimtaja mfungwa mwenzake aliyekuwa akimsisimua kwa stori zake kuwa ni Mama Rama, ambaye pamoja na mwanawe, Rama walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya mtoto wa kike.

Tayari Mama Rama na mwanawe wameshaachiwa huru na mahakama baada ya 
kuonekana hawana hatia, lakini Rama amepelekwa hospitali ya Mirembe ya mkoani Dodoma kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi. Mirembe ni hospitali maalumu ya wagonjwa wa akili.

Alipoulizwa ni kesi zipi zinazowakabili wanawake wengi waliofungwa jela, Kajala alisema nyingi zinatokana na makosa ya kutupa watoto na zingine chanzo chake ni wanaume. Alisema wapo wanawake waliohukumiwa vifungo vya miaka 30 jela baada ya wanaume zao kukamatwa kwa ujambazi.

"Wanawake wengi walikamatwa wakiwa na wanaume zao kwa makosa ya ujambazi, lakini si kweli kwamba walishiriki katika matukio hayo,"alisema Kajala.

Akizungumzia mazingira ya jela, Kajala alisema walikuwa wakifunguliwa saa 10 alfajiri kwa ajili ya kuhesabiwa na kunywa uji kabla ya kupangiwa kazi za kufanya. Alisema kila ilipofika saa 10 jioni, walitakiwa kwenda kulala na ilipofika saa tatu usiku kengele ya kuwazuia kuzungumza ilikuwa ikipigwa.

Alikanusha madai ya kuwepo kwa vitendo vya usagaji jela kwa kusema kuwa, wafungwa na mahabusu wanalala taa zikiwa zinawaka na wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa kike.

Kajala anakumbuka siku moja akiwa kwenye karandinga la polisi, akitoka mahakama ya Kisutu kurudishwa Segerea, alimuona msanii Barnaba Elias maeneo ya Mnazi Mmoja na kila mmoja alitamani kuzungumza na mwenzake, lakini ilishindikana.

Msanii huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema baada ya kunusurika kwenda jela, alifanyiwa tambiko na baba yake kwa kummwagia maji mwilini kabla ya kuingia nyumbani. Alisema siku hiyo alikesha akimzungumzisha mdogo wake usiku kucha. 

Pamoja na kukumbwa na matatizo hayo na mumewe, Kajala alisema ataendelea kumuheshimu kwa vile walifunga ndoa kanisani na kwa mujibu wa sheria za dini ya kikristo, hawapaswi kuachana.

"Siwezi kumshiti mume wangu, akitoka jela salama, atanikuta. Ndoa za kikristo hakuna kuachana,"alisisitiza.

Alisema pia kuwa, hawezi kuwachukia watu wake wa karibu waliomtelekeza wakati wa matatizo kwa vile kila kitu kinatokea kutokana na mipango ya Mungu.

Akizungumzia matarajio yake katika fani ya filamu, Kajala alisema anatarajia kutengeneza filamu itakayozungumzia maisha yake, ikiwa ni pamoja na matatizo aliyoyapata.

"Nimeandaa stori ya maisha yangu kupitia movi. Itazungumzia mambo yote yanayonihusu, tangu nilipokuwa na P Funky hadi nilipokamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka na maisha yangu ya jela,"alisema.

Kajala alisema katika filamu hiyo, atawatumia baadhi ya wasanii maarufu na chipukizi
kwa lengo la kuwapa uzoefu na kukuza vipaji vyao.

No comments: