MSANII anayetisha katika anga za muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein
Rashid, maarufu kwa jina la Hussein Machozi, amesema hayupo tayari
kupelekwa nchi za nje kwa ajili ya kufanya shoo za sebuleni.
Machozi amesema shoo za aina hiyo hazina maana yoyote kwa msanii kwa
vile hapati nafasi ya kuonyesha uwezo wake na kutimiza malengo yake
kimuziki.
Kwa mujibu wa Machozi, wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya nchini
wanaoalikwa kwenda kufanya maonyesho nje ya nchi, hawapati nafasi ya
kuutangaza muziki wao kimataifa kwa vile maonyesho hayo huwa ni kwa
ajili ya watu wachache.
Machozi alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa na
kituo cha televisheni cha Star TV kuhusu maendeleo na mustakabali wake
kimuziki.
"Kusema ule ukweli, sipo tayari kabisa kufanya shoo za sebuleni. Nasema
hivi kwa sababu wasanii wengi wa Tanzania wanaokwenda Ulaya, hufanya
shoo zao sebuleni kwa mtu ama kwenye kumbi ndogo za burudani kwa ajili
ya kuifurahisha familia ya mtu fulani ama mashabiki wachache,"alisema
msanii huyo, aliyewahi kutamba kwa vibao mbali mbali.
Machozi amevitupia lawama baadhi ya vyombo vya habari nchini, hasa redio
na televisheni kwa madai kuwa, vimekuwa vikiwabeba na kuwakuza wasanii
wachache wakati uwezo wao kimuziki ni mdogo.
Alisema baadhi ya vituo hivyo vimekuwa vikithubutu kupiga wimbo wa
msanii mmoja mara 10 hadi 15 kwa siku na hivyo kuzikosesha nafasi hiyo
nyimbo za wasanii wengine.
Msanii huyo aliyezaliwa Singida na kukulia mkoani Mwanza amesema wakati
umefika kwa mashabiki wa muziki nchini kupambanua uwezo wa wasanii na
ubora wa nyimbo zake badala ya kufuata upepo.
"Watu wa habari wakiamua kumtoa mtu fulani, wana uwezo wa kufanya hivyo
na wakafanikiwa. Lakini hao wanaopewa nafasi hiyo wanakuzwa tu, uwezo
wao ni mdogo,"alisema msanii huyo.
Ameielezea tabia hiyo ya kuwakuza wasanii wachache kuwa inachangia
kuwavunja nguvu wasanii chipukizi, ambao baadhi yao uwezo wao kimuziki
ni mkubwa.
Machozi alisema anamshukuru Mungu kwamba hadi sasa amefanikiwa kuteka
soko la muziki la Tanzania na tayari ameanza kubisha hodi katika nchi
jirani za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Alisema ameweza kufanya hivyo kutokana na mashabiki kuvutiwa na tungo
zake, ambazo zimekuwa zikigusa na kuelezea maisha ya kila siku ya jamii.
Hivi karibuni, Machozi alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari
akikanusha madai kwamba, amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii
nyota wa muziki wa kike wa Kenya, Avril.
Alisema amekuwa na uhusiano wa karibu na msanii huyo kama ilivyo kwa
wasanii wengine na kusisitiza kuwa, bado hajawa na mpenzi wa kudumu.
Msanii huyo mwenye sauti ya kubembeleza pia alikaririwa na vyombo vya
habari akisema kuwa, anafikiria kuhamishia shughuli zake za muziki
katika nchi jirani ya Kenya.
Machozi alisema amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa muziki wake
unakubalika na kuthaminiwa zaidi nchini humo kuliko Tanzania.
Msanii huyo, ambaye mara nyingi amekuwa akiweka kambi Kenya kila
anapojiandaa kutoa wimbo mpya, ameweka wazi kuwa anataka kuhama Tanzania
kwa vile kumejaa wanafiki wengi wa kimuziki.
Alipotakiwa kufafanua kuhusu madai yake ya kuwepo kwa unafiki mwingi wa
kimuziki bongo, Machozi alisema waandishi wa habari wamechangia kuwepo
kwa hali hiyo.
“Okay, watu wa media hawako free kabisa, yaani huwa wanafuata upepo wanapoanzisha wale wenye nguvu,”alisema msanii huyo.
“Yaani wakitaka kumtoa mtu wao na media zingine zinafuata, wala
hawashtuki kuwa analazimishwa atoke wakati kuna ngoma kibao kali
wanazipotezea ili mtu wao apite. Matokeo yake wanatoa ngoma moja inapata
umaarufu, baada ya hapo ni pumba tupu. Huwa inaniuma sana,” aliongeza
msanii huyo.
“Kwa Kenya mambo hayo hakuna kabisa. Kule kama ngoma ni kali,itatandikwa
hadi noma, ila kama ni mbaya, huwezi hata kuiskia,”alisisitiza msanii
huyo asiyekuwa na makeke.
”Nakubalika zaidi Kenya kwa sababu ngoma zangu ni kali na zina kichwa na
miguu, namaanisha wimbo unakuwa na stori ya kufuatilia na inasikilizika
na rika zote, nadhani hii ni sababu tosha sana,” alisema Machozi.
Hivi karibuni, msanii huyo alirekodi wimbo wake mpya unaojulikana kwa
jina la Addicted, akiwa amemshirikisha msanii anayetamba nchini Kenya
kwa sasa, Size 8.
Machozi alirekodi wimbo huo kwa ajili ya mashabiki wake wa kike na video ya wimbo huo imetengenezwa na Kampuni ya Ogopa DJs.
Hadi sasa, Machozi amerekodi nyimbo zaidi ya 15, lakini hakuna hata moja
iliyowahi kushinda tuzo ya muziki. Baadhi ya nyimbo hizo, ambazo
zimempatia umaarufu mkubwa ni pamoja na Kwa ajili yako, Mizimu, Kafia
ghetto, Nafasi, Jela, Unanifaa, Utaipenda na Wabongo ughaibuni.
Je, ni kwa nini amekuwa akijulikana zaidi kwa jina la Hussein Machozi?
"Nilipewa jina hili na mtangazaji mmoja wa redio RFA baada ya kuvutiwa
na nyimbo zangu, ambazo alikuwa akizielezea kwamba zina ujumbe wa
kusikitisha na kumtoa mtu machozi. Akawa anasema huyu mtu anafaa kuitwa
kwa jina la Hussein Machozi,"alisema.Inatoka kwa mdau.