skills za kitaa

Saturday, August 8, 2015

Ijue timu atakayochezea Kaseja



Baada ya kupata baraka za Shirikisho la Soka nchini (TFF) za kumruhusu kujiunga popote, kipa Juma Kaseja anajiandaa kutua Mbeya City.

Klabu hiyo ya Ligi Kuu imetangaza kuanza mazungumzo na mchezaji huyo ili aidakie timu yao kwa msimu ujao.
Katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema tayari mazungumzo ya awali yamekamilika na kilichobakiwa ni kumalizana na mchezaji huyo ili awe mali yao, wakiamini ataisaidia kwa uzoefu alionao.
Awali ilikuwa ikidaiwa kuwa, kipa huyo anajiandaa kutua Mwadui Shinyanga na pia ikielezwa anasakwa na kocha Patrick Liewig wa Stand United baada ya kukatisha mkataba wake na Yanga.
Hata hivyo Mbeya City imesisitiza kuwa kipa huyo ataidakia timu yao kama mambo yataenda sawa ikizingatiwa kuwa ilishamtema aliyekuwa kipa wao namba moja David Burhan aliyetua Majimaji ya Songea iliyorejea Ligi Kuu.
“Lolote linawezekana, tayari kikosi kina wachezaji 25 lakini kunahitaji la mchezaji mmoja ambapo kocha amependekeza nafasi hiyo kujazwa na kipa na tunaona Kaseja atatufaa sana.
“Hatuna shaka na kiwango chake ni kipa mzoefu,” Kimbe alisisitiza.
Mwanaspoti ilipomsaka Kaseja, kipa huyo alikiri kufanya mazungumzo na Mbeya City na kueleza huenda akaichezea wakimalizana.
“Ni kweli nimeshafanya mazungumzo na Mbeya City ili kusajiliwa huko. Mbeya City ni timu sahihi kwangu na ni timu nzuri ambayo inaleta ushindani. Pia tunafahamiana na kocha Mwambusi toka siku nyingi na niliwahi kuwa naye Moro United,” alisema Kaseja.

No comments: