skills za kitaa

Sunday, September 29, 2013

Katiba ni Mwafaka wa Kitaifa. Viongozi zungumzeni


Zitto Kabwe.
Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu muswada wa sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya sheria ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011.

Mjadala na upitishaji wa sheria hii uliweka rekodi ya pekee katika nchi yetu kwa vitendo vya kihuni kutokea Bungeni ambavyo nisingependa kuvirejea kutokana na aibu kubwa ambayo Bunge liliingia.
Kiukweli kuna sintofahamu katika nchi kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya. Hii imechangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande zote mbili, wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo.

Masuala ya Tume imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu wanapatikanaje na kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka kwa viongozi kukaa na kuzungumza.

Haya sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka labda kuwe na nia mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio suala la kufanyia siasa. Katiba ni uhai wa Taifa.
Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo lingependa pasiwe na katiba mpya ya Wananchi. Kuna kundi lingine ambalo lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka mingine zaidi ili kuweza kupata Katiba bora. Kuna kundi la Wabunge ambao kwa chinichini wanataka mchakato uendelee, uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge.

No comments: