
NGULI wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amesema,
anajivunia kuweka historia ya kufanya onyesho, ambalo mashabiki wamelipa
kiingilio kikubwa ili kumshuhudia.
Diamond ameeleza kupitia mtandao wake kuwa, katika maisha yake, hajawahi
kufanya onyesho, ambalo mashabiki walilipa zaidi ya sh. 20,000.
Katika onyesho hilo lililofanyika wiki iliyopita kwenye ukumbi wa klabu
ya Safari Carnival mjini Arusha, kiingilio kilikuwa sh. 150,000 kwa mtu
mmoja.
"Kiukweli namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuweza kufanikisha onyesho
hilo,"alisema msanii huyo, ambaye amewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki
za Kilimanjaro.
"Huwezi kuamini, licha ya kiingilio kuwa kikubwa, mashabiki walifurika
pasipo hata mimi kutegemea. Kiukweli, ilinifariji sana,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Diamond, wingi wa mashabiki hao ulidhihirisha kwamba
watanzania wanathamini na kujali vipaji vya wasanii wao tofauti na
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
"Zamani shoo ya kiingilio kikubwa ilikuwa mpaka msanii atoke nje ya
nchi. Hali hii inanipa changamoto ya kuzidi kufanya vizuri, kujituma na
kuwa mbunifu zaidi,"alisema.
Diamond alisema moja ya mipango yake ya baadaye kimuziki ni kuitangaza Tanzania kimataifa.
Aliushukuru uongozi wa Safari Carnival na mashabiki wote wa muziki wa Arusha waliojitokeza kushuhudia onyesho hilo.